Thursday, July 12, 2012

SMZ KUANZISHA MFUKO WA BIMA YA AFYA ILI KUWASAIDIA WANANCHI WAKE.

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar

Serikali ya Zanzibar inatarajia kuanzisha mfuko wa bima ya afya ili kuweza kuwaondolea usumbufu wa tiba wananchi wake .

Hayo yamesemwa katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya wakati akijibu suala la Jaku Hashim Ayoub Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni aliyetaka kujua uanzishwaji mfuko wa bima ya afya kwa Zanzibar.

Dk. Sira alisema kwamba uanzishwaji wa huduma ya bima ya afya kwa Zanzibar ni tayari na hivi sasa iko katika hatua za awali za kufanya tafiti za kuweza kujua utayari wa uwezo wa wananchi .

Alisema kuwa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeshawapatia mafunzo wafanyakazi wa Wizara ya afya Zanzibar juu ya jinsi ya kuendeleza mfuko huo kwa hospitali zote za serikali Binafsi na NGO kwa unguja na Pemba .

Dk. Sira alisema mfuko wa bima ya afya ya Zanzibar umeshafungua ofisi yake na kuweza kuwajiri wafanyakazi wake wakiwemo daktari, muhasibu, na dereva .

Aidha alisema kuwa tumaini ni kwamba mfuko huo utafanyakazi vizuri kwa lengo la kuziwezesha hospitali za Serikali za Unguja na Pemba ziweze kunufaika na huduma hiyo.

Akieleza dhamana ya uazishwaji wa mfuko huo alisema itasimamiwa na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kwa upande wa mfuko wa bima wa taifa,alisema tayari umeanza kufanya kazi zake Zanzibar kuanzia mwaka 2007 na una jumla ya wanachama 5,393 ukichanganya pamoja na familia zao idadi inafikia 28,044 wanafaidika na mfuko huo.

No comments:

Post a Comment